Wasichana wengi wanaojihusisha na maswala ya ngono katika umri mdogo
wanakabiliwa na ongezeko la uwezekano wa kupata saratani ya mlango wa
mji wa mimba (cervical cancer). Shingo ya mlango wa mji wa mimba ambayo
haijakomaa inapokutana na misukosuko ya ngono hudhoofika na kupoteza
nguvu za kukabiliana na mashambulizi ya virus vya Human Papilloma –
(HPV) ambao husababisha saratani hiyo mapema au baadaye sana.
Virusi hawa huambukiza kwa njia ya kujamiiana na wanaume hata kama
mwanaume atakuwa amevaa kondomu wakati wa kufanya tendo la ngono na
msichana. Saratani hii ni tatizo kubwa la kiafya linaloongoza kwa vifo
vya wanawake vitokanavyo na ugonjwa wa saratani katika nchi
zinazoendelea. Saratani hii kwa kawaida huwapata wanawake wengi ambao
huanza kufanya tendo la kujamiiana katika umri mdogo, miaka michache
baada ya kuvunja ungo.
Wasichana na wanawake wenye wapenzi wengi, au wenye wapenzi wa kiume
ambao wana mtandao mkubwa wa wapenzi wengine wengi, huwa katika hatari
kubwa ya kupata maambukizi ya virusi wanaosababisha ugonjwa wa saratani
ya mlango wa kizazi.
Kwa bahati mbaya sana wasichana wengi hupata maambukizi ya virusi hawa
kwa kufanya ngono kwa mara ya kwanza, hata kama ni mara moja tu. Tatizo
jingine kuhusiana na maambukizi ya virusi hawa ni kwamba, msichana
anaweza kuishi na virusi hawa bila habari kwa miaka 10 hadi 15 hivi
ndipo madhara yake yanapojitokeza kwa wazi.
Tatizo jingine linalowakabili wasichana wadogo wanaoendekeza ngono ni
ugumba wakati watakapo hitaji kuzaa. Magonjwa mengi ya ngono hushambulia
mirija ya uzazi na kusababisha mirija hiyo izibe. Mirija ya uzazi
inapoziba, hushindwa kupitisha mayai kwa ajili ya kutunga mimba pale
msichana atakapohitaji kupata watoto hapo baadaye.
Magonjwa ya ngono kwa wasichana pia husababisha maumivu makali na kuugua
hasa pale tumbo la chini linaposhambuliwa. Msichana hupata ugonjwa wa
mwanamimba yaani uambukizo katika mji wa mimba na wakati mwingine katika
njia ya mkojo. Hii pia huambatana na maumivu makali wakati wa kukojoa.
Magonjwa mengine katika kundi hili la magonjwa mengi mbalimbali,
husababisha madhara makubwa na ya muda mrefu. Kaswende inaweza
kusababisha ugonjwa wa moyo na akili hasa pale msichana anapochelewa
kupata matibabu sahihi. Magonjwa haya pia yanaweza kukaa mwilini kwa
muda mrefu bila kuonyesha dalili huku yakiendelea kudhuru afya ya
msichana.
No comments:
Post a Comment