Siku hizi ngono kabla ya ndoa hutazamwa na vijana wengi kama jambo la
kawaida.Vijana wa kike na wa kiume hawahisi hatia yoyote ya kuwa na
uhusiano wa kingono katika umri mdogo. Kwa kufanya hivi vijana hupoteza
mwelekeo kwa kuishi kiholela bila ya kuwa na mwongozo unaongoza maisha
yenye mafanikio sasa na baadaye. Uwezo, fursa na bahati ya vijana kwa
ajili ya maisha bora hupotea bure. Vijana hufikiria kuwa ngono ndilo
jibu na ufumbuzi wa hali ngumu wanayokabiliana nayo wakati wa balehe na
kupevuka. Wengi wao hupungukiwa uwezo wa kutabili nini kitatokea baadaye
kama matokeo ya ngono kabla ya ndoa.
Wasichana wanaojiingiza katika mahusiano ya kingono kabla ya ndoa na
katika umri mdogo huweka rehani uaminifu, afya na uvumilivu wao wa hisia
kuhusu mahusiano ya kingono wakati watakapo ingia ndani ya ndoa hapo
baadaye.Vijana wengi hawaelewi kuwa ngono haramu huzaa wivu, tuhuma
mbaya na majanga ya kijamii. Hufanya mwenzi kumfikiria msichana kuwa ana
udhaifu wa kimaadili na hali hii hutia alama katika hisia za mwenzi
kuhusu hali ya uaminifu wa mwenzake hasa pale anapokuwa mbali naye.
Tafiti kadha wa kadha huonyesha kuwa wasichana wasiothamini umuhimu wa
kujitunza, kujilinda na kubakia waaminifu kabla ya ndoa, wana uwezekano
mara dufu wa kufanya ngono nje ya ndoa baada ya kuolewa ikilinganishwa
na wale wanaojitunza na kuanza ngono ndani ya ndoa. Uzoefu pia
unaonyesha kuwa wasichana wengi wanaoanza ngono kabla ya ndoa, maisha
yao ya baadae huwa magumu kutokana na kuacha masomo au kuzaa hovyo ovyo
bila mpangilio. Wengi hujikuta wakizaa na wanaume wengi tofautitofauti
na kusababisha malezi ya watoto kuwa magumu.
Wasichana wengi hufikiri kuwa ngono kabla ya ndoa ndio njia pekee ya
kujenga na kudumisha uhusiano wa kimapenzi na wavulana. Hii si kweli na
huenda msichana na mvulana wanaotamaniana kingono hutazamana kwa
mitazamo inayotofautiana kabisa mara baada ya tendo la ngono. Ni vigumu
kutabiri nini kitatokea baada ya mvulana kutosheleza tamaa yake ya ngono
kwa mara ya kwanza.
Huenda mvulana akamwona msichana havutii tena kimahaba na kumchukia
sana. Huenda msichana pia akapata athari za kisaikolojia na kupata hisia
za kunyanyaswa kijinsia au kutumiwa kama chombo cha kustarehesha
wanaume kingono. Na huenda akajichukia kwa udhaifu na kujirahisisha
aliko onesha. Hii mara nyingi hutokea pale msichana anapokataliwa na
mvulana baada ya kupata mimba.
Mbali na athari za kisaikolojia na kijamii, ngono katika umri mdogo
kabla ya ndoa pia inazo hatari za kiafya katika mwili wa msichana.
Tishio kubwa kwa wasichana ni maambukizi ya magonjwa kama vile virusi
vya UKIMWI, kansa ya mlango wa mji wa mimba na magonjwa mbalimbali
yaambukizayo kwa njia ya ngono.
No comments:
Post a Comment