Magonjwa ya ngono ni maambukizi yanayosambazwa kwa njia ya tendo la
ngono au kujamiiana. Magonjwa haya kwa karne nyingi yamejulikana kama
nyororo la maangamizi au bomu la kibaiolojia. Hii ni kutokana na ukweli
kuwa ukiona mgonjwa mmoja mwenye tatizo la ugonjwa wa kuambukiza kwa
njia ya ngono basi ni muhimu kutambua kuwa kuna mtu mwingine nyuma yake
ambaye ana tatizo hilo pia.
Kwa kawaida wasichana huwa katika hatari kubwa zaidi ya kupata magonjwa
ya ngono kama watajiingiza katika vitendo vya kujamiiana. Sababu kubwa
zinazowaweka katika hatari ni ile hali ya kushindwa kuamua namna ya
kufanya ngono kwa tahadhari, maumbile ya kike kama mpokeaji na
kutokukomaa kwa shingo ya mji wa mimba nazo ni sababu zingine
zinazoongeza hatari.
Magonjwa mengi ya ngono husababishwa na bakteria, virusi, kuvu (fungus),
protozoa na parasaiti. Magonjwa yasababishwayo na bakteri ni kama vile
kisonono, mitoki (Granuloma inguinale na Chancroid), kaswende na
klamydia. Magonjwa kama vile malengelenge (Herpes simplex), molluscum
contageosum, viotea (warts), virusi vya UKIMWI na saratani ya mlango wa
kizazi (HPV infection) haya hutokana na virusi. Magonjwa yasababishwayo
na kuvu ni kama vile kandidiasisi ambayo huambatana na muwasho sehemu za
siri. Magonjwa yaletwayo na protozoa kama vile Trikomoniasisi pia
husababisha muwasho sehemu za siri na hutokwa kwa majimaji machafu yenye
harufu mbaya hasa kwa wanawake. Upele na chawa wanaokuwa kwenye nywele
za kinenani haya pia ni magonjwa ya ngono yanayosababishwa na parasaiti.
Dalili za magonjwa ya ngono hujitokeza kwa njia na dalili nyingi. Wakati
mwingine magonjwa haya hayatokezi dalili zozote na pia mgonjwa anaweza
kupata maambukizo ya magonjwa mawili au zaidi kwa wakati mmoja
anapotenda tendo la ngono. Hatari kubwa zaidi inayoambatana na magonjwa
haya ni kutokuwepo kwa dawa zinazotibu baadhi ya magonjwa haya kama vile
UKIMWI.
No comments:
Post a Comment